UMENUNULIWA

Bwana Yesu Asifiwe! 

 Biblia inatufundisha jambo la msingi sana—kila aliyeokoka amenunuliwa.
"Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu." 1 Wakorintho 7:23
Hili ni suala la umiliki:
Nani anakumiliki? 
 Kama tulinunuliwa, basi ni dhahiri kuwa kulikuwa na aliyehusika kukuuza, na kuna mwingine aliyekununua

Hii pia inamaanisha wazi kuwa wewe si mali yako mwenyewe. 
Fikiria gari—halijinunui lenyewe. Linahitaji mmiliki. 
Vivyo hivyo, chochote kinachoweza kununuliwa, hakiwezi kujimiliki chenyewe. 

Hili linabeba uzito mkubwa sana: Haijalishi umeokoka au hujaokoka—kila mtu yuko chini ya umiliki. Na ikiwa Mungu ndiye aliyekununua, basi kuna aliyekuuza. Na hapa ndipo tunaona ufahamu mdogo wa shetani:
 
Alimuuza mwanadamu pasipo kujua kuwa anapoteza kabisa haki ya umiliki Juu ya mwandamu! 
Shetani alisaini mkataba huu alipomtumia Yuda kumsaliti Yesu—akidhani anashinda, kumbe anauza mali aliyokuwa anaimiliki. 

 Uthamani Wako ni wa Kiasi Gani? 

Kama gari linavyothaminiwa kwa bei inayotumika kulinunua, ndivyo thamani ya mwanadamu inavyopimwa kwa kile Mungu alikitoa kumnunua. 

Naomba usipime thamani yako kwa kiwango cha utakatifu wako. Thamani yako haibadiliki kwa sababu umeanza kuishi maisha ya utakatifu—kwani ulinunuliwa ukiwa mdhambi. 

Sasa, Je! Thamani Yako ni Kiasi Gani? 
"Hamjui ya kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe." 1 Wakorintho 6:19 


 "Maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu." 1 Wakorintho 6:20



 "...mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe." Matendo 20:28

Thamani hiyo ni damu ya Yesu Kristo mwenyewe. Kumbuka, damu ni uhai wa mtu. Kutoa damu ni kutoa maisha. 

Kwa hiyo kwa mantiki hiyo, wewe una thamani mbele za Mungu sawa na Yesu mwenyewe. 

Mungu alikulipa thamani ya juu mno, wakati wewe ni ‘used car’—mchafu, mwenye dhambi, na umeharibika. Lakini bado alikununua. 

Na baada ya kununua, ndipo alianza kukutengeneza. Ooh Yesu! Ni upendo wa ajabu kiasi gani! Wote Ni Mali ya Mungu – Tumeokoka au La Tukiwa na ufahamu huu wa thamani ya mwanadamu, hatutahubiri kwa hukumu, bali kwa rehema. 

Wale walioko mitaani bado wanafanya dhambi ni mali ya Mungu tayari. Damu ya Yesu imeshatolewa. Mtu anapookoka si kwamba ndio ananunuliwa siku hiyo—manunuzi yalifanyika tayari pale Kalvari. 

Roho ya mwanadamu si haki ya shetani tena. Damu ya Yesu ni kama hundi inayoonesha: “umelipiwa.” 

Ndio maana shetani anaogopa damu ya Yesu—kwa sababu ni ushahidi kwamba hafai tena kuwa mmiliki. Sasa basi, tunapohubiri, tunaomba kupitia damu ya Yesu kudai nafsi ambazo zilinunuliwa lakini bado hazijarudi nyumbani. 

 
Hitimisho
Wewe ni mali ya Mungu. Ulinunuliwa kwa thamani kuu—damu ya Yesu Kristo mwenyewe. Acha ukweli huu ukutie moyo, ukuinue, na ukusukume kuishi maisha ya kumtukuza Mungu. Na zaidi ya yote, tuelewe thamani ya roho ya mwanadamu—ili tuhukumu kidogo na tuhubiri zaidi. 

Ubarikiwe sana kwa somo hili.

Comments

Yaliyopendwa zaidi

SIRI YA WOKOVU 1

NJIA TANO ZA KUFANIKIWA